HOTUBA
YA MKE WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
MHESHIMIWA
MAMA
SALMA KIKWETE
AKIZINDUA
MRADI WA MAFUNZO KWA SEKTA YA GESI NA MAFUTA YA PETROLI
CHUO
CHA MAFUNZO NA ELIMU YA UFUNDI STADI, LINDI,
10
OKTOBA, 2013
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi -
Mheshimiwa Philipo Mulugo (Mb)Mkuu wa Mkoa wa Lindi -
Mheshimiwa Ludovick Mwananzila
Mkuu wa wilaya ya Lindi;
Mkurugenzi Mkuu VETA – Eng Zebadiah S. Moshi
Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya ufundi – Leah Lukindo
Meneja wa Tanzania wa British Gas – Kate Sullam
Mkurugenzi wa Tanzania wa Volunteer Service Organisation – Jean Van Wetter
Mkurugenzi wa VETA kanda ya kusini mashariki – Wilhard Soko
Wakuu wa vyuo vya VETA Lindi na Lindi
Washirika wengine wa Maendeleo;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Waheshimiwa Wabunge;
Viongozi wa Serikali;
Viongozi wa Dini;
Waalimu;
Wageni Waalikwa;
Wanafunzi;
Mabibi na Mabwana:
Ndugu Wananchi:
Awali
ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha mahali hapa katika
kutekeleza majukumu ya Kitaifa kwa jamii na hasa vijana ambao ndio kundi lengwa
kwa siku ya leo.
Ninayo
furaha kubwa pia kuja hapa Lindi kuzindua awamu ya pili ya Mradi wa Mafunzo na
Elimu ya Ufundi Stadi kwa ajili ya Sekta ya Gesi na Mafuta ya Petroli wenye
madhumuni ya kuimarisha ajira kwa vijana kupitia ufundi stadi Lindi (Enhancing Employability through Vocational
Training – EEVT).
Ninapenda
kuanza kwa kutoa shukurani na pongezi zangu za dhati na kipekee kwa Kampuni ya
British Gas ya Uingereza, Voluntary Services Organisation (VSO Tanzania) ya
Uingereza, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, VETA, na wote walioshiriki kufanikisha
kuanzishwa na kuendelezwa kwa Mradi huu. Ninapenda
pia, kuwashukuru washirika wengine wa maendeleo ambao wameshiriki kwa namna
moja au nyingine katika kufanikisha kuanza kwa Mradi huu hususan Serikali ya
Uingereza kupitia Idara yake ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID), British Council,
Serikali na wananchi wa Mkoa wa Lindi .
Naipongeza
pia Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi chini ya Mwenyekiti wake Prof. Idrissa Bilal Mshoro pamoja
na Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
inayoongozwa na Eng. Zebadiah Moshi, kwa kuhamasisha uanzishwaji wa Mradi huu
na sasa tuko katika hatua ya pili ya uzinduzi wa mradi kwa mkoa wa Lindi,
hongereni sana. Nina imani kubwa kuwa wataendelea kufanya kazi nzuri ili
malengo ya Mradi huu yaweze kutimia. Pia, ninatambua kazi kubwa iliyofanywa
katika awamu ya kwanza ya mradi huu katika chuo cha ufundi VETA Mtwara na sasa
awamu ya pili kwa VETA Lindi.
Ndugu Wananchi;
Natambua
kuwa mradi kama huu tayari umeanza kwa mkoa wa Mtwara katika chuo cha ufundi
VETA Mtwara ambapo Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Gharib Bilal
alizindua mradi huo pale Mtwara mwishoni mwa mwaka jana 2012. Ninajisikia
mwenye furaha kufanya vivyo hivyo katika uzinduzi huu kwa mkoa wa Lindi
nikiamini vijana wa Lindi na maeneo mengine watafaidika na fursa hii. Serikali
itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote wa maendeleo kupitia vyombo husika
kama VETA ili kujenga mazingira mazuri ya kutoa ajira.
Ndugu wananchi
Kwa
namna ya kipekee sana naomba nitoe msisitizo nikiwa kama mama lakini pia kama
mmoja wa wana-maendeleo katika Mkoa wa Lindi. Ninatambua changamoto za mtoto wa
kike katika kupata elimu kwa ngazi zote. Ni matumaini yangu kuwa fursa hii ya
mradi huu itatoa mwanga kwa mtoto wa kike. Nitoe wito kwa wazazi na walezi
kuwajengea mazingira mazuri watoto wa kike ili washiriki sawa na watoto wa
kiume katika kunufaika na mradi huu. Wataalamu wanasema; ukimuelimisha mtoto wa
kike umeelimisha jamii nzima. Tutumie fursa hii vizuri ili vijana wetu wapate
ujuzi wenye viwango vya kimataifa na hivyo kushindana katika soko la ajira la
sasa.
Ndugu wananchi
Nafurahi
kuzindua Mradi huu nikiwa na matumaini makubwa kwamba Watanzania hasa vijana sasa
tumepata moja ya ufumbuzi wa changamoto ya ajira hasa kwa vijana, kwa kutumia
fursa ambazo zimejitokeza katika Sekta hii.
Ndugu wananchi na Wageni Waalikwa,
Baada
ya kusema haya machache, sasa natangaza rasmi kuwa nimezindua rasmi Mradi huu
wa Mafunzo na Elimu ya Ufundi Stadi kwa Sekta ya Gesi na Mafuta ya Petroli kwa
chuo cha ufundi stadi Lindi.
Ahsanteni
sana kwa kunisikiliza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni